Akiendelea na siku ya pili ya ziara yake nchini Uganda, Papa Francis ametembelea madhabahu takatifu ya nchi hiyo, ambako aliongoza misa mbele ya waumini laki tatu.
Katika hotuba yake aliwahimiza Waganda kuheshimu historia ya mashuja katika maisha yao ya kila siku.
Baada ya kutembelea madhabahu ya mashuja ya Namugongo siku ya Jumamosi ambako mashuja 45 wa karne ya 19 waliteswa na kuchomwa wakiwa hai kwa kukataa kubadili Imani yao ya kidini, Papa Francis aliwahimza waganda kuwatumikia wenzao kwa moyo wa ubinadamu na unyeyekevu, hasa wazee, maskini na waloachwa au kupoteza familia zao, akisema ndio njia pekee wanayoweza kudai wanamtumikia mwenyezi mungu.
Iris Babiirye anasema atachukulia somo hilo moyoni kwa dhati.
Akongoza misa hiyo katika kanisa katoliki la Namugongo, Papa Francis amewataka viongozi wa kisiasa kutumia fursa walio nayo kuwahudumia raia na wala sio kuonyesha ubabe wao kwa kuwadhulumu wenzao, akieleza kwamba madaraka ya dunia hayana amani ya kudumu.
Hapo tena mkuu wa Kanisa la kikatholiki alisafiri hadi mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa ndege usotumiwa wa Kololo mjini Kampala na kukaribishwa kwa shangwe na karibu vijana 150 000.
Akiwa kwenye uwanja huo alimsikiliza msichana ambae amegeuka kuwa mwanaharakati aliyezaliwa na virusi vya HIV na mwaname aliyetekwa nyara wakati mmoja na kundi la Lord Resistance Army na kuweza kutoroka na baadae kusoma na kupokea shahada ya chuo kikuu.
Papa Francis aliwambia vijana kwamba Imani inaweza kuwasaidia kukabiliana na matatizo yote ya maisha
Ujumbe ambao Susan Labwot anasema, ni muhimu kwa vijana wa nchi yake.
“Huo mfano mzuri kwamba Papa amewasili nchini mwetu katika wakati huu muhimu ili kuwapatia motisha vijana, vijana wanapata muongozo fulani kutoka kwa Papa.”
Na wengine wengi kama Bernard Otonga, wanamatumaini ujumbe wa Amani na maridhiano wa Papa utaendelea hadi mwakani wakati Waganda wanajitayarisha kwa uchaguzi wa Rais.
“Mapema mwakani tuna uchaguzi na tuna amini Papa atatuombea ili kuwepo na uchaguzi wa Amani nchini.
Papa aliendelea na ziara yake yenye shughuli nyingi Jumamosi kwa kukutana na wagonjwa, wazee na walemavu katika nyumba ya wahisani pamoja na kukutana na viongozi kanisa la Kikatholiki na viongozi wa dini nyenginezo nchini humo.
Kiongozi huyo anapangwa kuondoka Kampala Jumapili kwa hatua ngumu ya ziara yake ya Afrika huko Jamuhiri ya Afrika ya Kati ambako ghasia za kidini zimesababisha vifo vya maelfu ya watu.