Rais John Magufulu wa Tanzania amelifungua rasmi bunge la kumi na moja la taifa hilo la Afrika Mashariki akiahidi kutekeleza ahadi alizotowa wakati wa kampeni za uchaguzi.
Aidha rais aliwapongeza wabunge waliochaguliwa pamoja na jinsi uchaguzi ulivyofanyika hasa namna tume ya uchaguzi ilivyotayarisha na kusimamia uchaguzi mzima kwa msaada mkubwa wa vikosi vya usalama.
Kiongozi huyo amesema hivi sasa wananchi wanasubiri kuona madai yao yamesikilizwa na kutekelezwa na hivyo wanahitaji uwajibikaji wa watu wote.
"Sisi sote watatupima kwa namna tutakavyo kidhi kiu na matarajiyo yao. Na sote tuliahidi kuwatumikia wananchi.Na kutokana na utumishi wetu kwao tuweza kutatua matatizo mbali mbali."
Rais Magufuli aliorodhesha malalamiko yote aliyoyasikia wakati wa kampeni za uchaguzi kuanzia ulaji rushwa hadi haki za kiaria na utendaji kazi. Lakini muhimu zaidi alisema ni kulinda amani iliyodumu katika kipindi kizima cha uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Pamoja na kero hizo zote kiongozi wa utawala wa awamu ya tano ya Tanzania amesema atalinda mungano na kuuimarisha.
Rais Magufuli anasema donda kuu alilolikemea wakati wa kampeni ni ulaji rushwa na ufisadi, na ana ahidi kupambana na hali hiyo kwa dhati.
Vipaumbele vya serikali anavyotarajia kuviunda vitakuwa ni kupunguza urasimu, ili kuongeza kasi katika utekelezaji wa maamuzi na miradi ya serikali, kurejesha nidhamu ya serikali na utumishi wa umma.
Hatimae Rais Magufuli aliahidi kuimarisha ushirika na uhusiano wa kikanda na kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania.
Kabla ya kiongozi huyo kuwasili na hadi kuingia bungeni wabunge wa upinzani UKAWA walikua wanapiga makelele wakiimba "Maalim Seif, Maalim Seif", wakieleza upinzani wao kutokana na uhalali wa Rais Maguful;i bila ya mzozo wa Zanzibar kutanzuliwa.
Kiongozi wa chama cha NCCR mageuzi katika mungano wa UKAWA James Mbatia anasema wanapinga kwa sababu uchaguzi haujakamilika bila ya kutanzua mzozo wa Zanzibar.