Vuguvugu la mungano wa vyama sita vya upinzani na asasi za kiraia Burundi limetowa wito wa kuwepo utulivu na amani wanaposubiri kusikiliza uwamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza, ikiwa atagombania kiti chake kwa mhula wa tatu au la.
Warundi na dunia nzima wanasubiri kwa hamu matokeo ya mkutano mkuu wa chama tawala cha CNDD-FDD utakaofanyika Jumamosi April 25 mjini Bujumbura, ambapo inatazamiwa chama hicho kitamtangaza mgombea wake kwa ajili ya uchaguzi wa rais wa mwezi wa June.
Akizungumza na Sauti ya Amerika kiongozi wa vuguvugu hilo jipya la kupinga mhula wa tatu wa Rais Nkurunziza, Chauvineau Mugengezo anasema vyama vya upinzani havitakubali kwa kiongozi huyo kugombania kwa mhula wa tatu kwa sababu katiba haimruhusu kufanya hivyo.
Bw Mugengezo, anasema pindi Rais Nkurunziza atatangaza anagombania kwa mhula wa tatu basi watatowa wito wa warundi wote kushuka barabarani kwa njia ya amani na kupinga uwamuzi huo, "tunaomba Mola ampatiye buisara abadili uwamuzi wake na kuinusuru nchi hii kutokana na maafa mengine."