Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 19, 2024 Local time: 04:53

Wachumi, wasomi watoa wito kwa serikali kuhahikisha mafanikio yanapatikana mradi wa SGR


Uzinduzi wa mradi wa SGR Tanzania. Picha na mwandishi wetu Amri Ramadhani
Uzinduzi wa mradi wa SGR Tanzania. Picha na mwandishi wetu Amri Ramadhani

Baadhi ya wachumi na wasomi nchini Tanzania weitaka serikali kuhakikisha mradi wa reli ya umeme SGR unaleta manufaa kwa wananchi wa matabaka yote kwa kutoa huduma zenye bei nafuu huku wakishauri mradi huo ujikite katika usafirishaji wa mizigo ili kuhakikisha unarudisha uwekezaji uliofanyika.

Kwa mara ya kwanza leo, mradi wa Reli ya Umeme (SGR) unafanyiwa majaribio kwaajili ya kuanza kazi kipande cha kwanza cha kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro. Wachumi na wasomi nchini wanaweka msisitizo kwenye umuhimu wa mradi huu kuleta manufaa kwa wananchi wa kila tabaka, hasa kupitia utoaji wa huduma zenye bei nafuu.

Mhandisi Mohammed Mtambo kutoka Dar es Salaam, ambae ni mdau wa maendeleo, ametoa wito kwa serikali kuchukua mradi huo kama huduma kwa wananchi na si biashara.

"Serikali iizingatie hii kama huduma na sio kama biashara na isitarajie faida ya muda mfupi. Hii ni huduma na serikali inapaswa kutoa huduma hii kwa gharama ya chini angalau kwa hatua za awali," amesisitiza Mtambo.

Mradi wa Reli ya Umeme (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, wenye urefu wa kilomita 300, ulianza ujenzi wake mnamo Mei 2, 2017, na kugharimu Trillion 2.7 za Kitanzania. Hii ni hatua muhimu kwa maendeleo ya Tanzania na inaleta matumaini kwa wananchi kuhusu kuongezeka kwa uchumi wao

Uzinduzi wa mradi wa SGR Tanzania. Picha na Mwandishi wetu.
Uzinduzi wa mradi wa SGR Tanzania. Picha na Mwandishi wetu.

Hata hivyo, Ntui Mposiani, Mhadhiri wa Uchumi na Biashara, kutoka Chuo cha Mtakatifu Agustine Mwanza anasisitiza kwamba manufaa yanapaswa kuendana na ukubwa wa mradi, hususan kupitia usafirishaji wa mizigo.

"Mizigo itakayosafirishwa inaweza kuleta pesa nyingi zaidi ambazo zitatumika kwa manufaa ya wananchi wote bila kuangalia anapanda treni au hapandi treni," anasema Mposiani.

Nae Eugene Follonja, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Agustine Mwanza, anasisitiza umuhimu wa kuajiri watu wenye sifa na weledi kusimamia mradi huu.

"Waajiriwe watu ambao watakuwa wanaendesha hilo shirika wawe na sifa, wasiwe ni ndugu tu wa haya matabaka kwasababu tu ni ndugu. Wawe na sifa za kuweza kuendesha, lakini pia matabaka yote yajisikie hiyo reli ni yao isiwe reli ya watu fulani wengine wajione haiwahusu waanze kuihujumu," anasisitiza Follonja.

Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi, ametoa uhakika kwa Watanzania kwamba huduma za SGR kati ya Dar es Salaam na Morogoro zitaanza ifikapo Julai mwaka huu.

“Ule wasiwasi uishe Rais Samia Suluhu Hassani wakati akizungumza na Watanzania katika kuukaribisha mwaka mpya alisema shirika la reli hadi kufikia mwezi wa saba huduma ziwe zimeanza kwahiyo shirika halitofanya kosa kwenye maagizo ya Rais litaanza huduma hizo maana yake kufikia mwezi wa saba sio majaribio tena bali Watanzania wamekwenda safari wamerudi” amesema Matinyi

Hata hivyo, wachumi na wasomi wanaendelea kutoa ushauri, wakiitaka serikali kuhakikisha miundombinu ya bandari na reli inaunganishwa kwa ufanisi ili kuchochea uchumi kwa njia bora zaidi.

Imeandaliwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika

Forum

XS
SM
MD
LG