Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Septemba 25, 2024 Local time: 09:28

Tunataka nafasi za kudumu kwenye Baraza la Usalama la UN- Afrika yasema


Rais wa Afrika Kusini akitoa hotuba yake kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York. Septemba 19, 2023. Picha ya maktaba.
Rais wa Afrika Kusini akitoa hotuba yake kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York. Septemba 19, 2023. Picha ya maktaba.

Nigeria imejiunga kwenye orodha kubwa ya viongozi wa Afrika waliopo kwenye mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea mjini New York, kutaka mageuzi kwenye Baraza la Usalama.

Kwa muda mrefu Afrika imekuwa ikiitisha nafasi za kudumu kwenye Baraza hilo. Hata hivyo kama Timothy Obiezu anavyoripoti, baadhi ya wachambuzi wa kieneo hawaamini kuwa hilo linawezekana. Wakati kikao hicho cha 79 cha UN kikiendelea New York, viongozi wa dunia wanatarajiwa kufikia maelewano kuhusu mageuzi yanayohitajika.

Hata hivyo kibarua kikubwa kipo upande wa Afrika, bara ambalo kwa muda limekuwa likiitisha walau viti viwili vya kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja huo. Pembeni mwa mkutano huo, Jumatatu waziri wa Ulinzi wa Nigeria Mohammed Badaru, aliomba kufanyika kwa mageuzi kwenye Baraza la Usalama, akisema kuwa hatua hiyo ingeleta haki na ushirikishwaji zaidi.

Nigeria siyo nchi pekee inayoitisha mabadiliko hayo. Mwishoni mwa wiki, rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alisema kuwa, “Kuweka usalama wa dunia mikononi mwa watu wachache, wakati wengi wakiwa wanakabiliwa na vitisho, siyo haki wala hali endelevu.

Rais wa Kenya William Ruto pia alilalamikia mfumo wa kimataifa uliopo, akisema kuwa haufanyi kazi ipasavyo. Mwaka 2005, Umoja wa Afrika kwenye makao yake makuu nchini Ethiopia, ulifikia makubaliano ya Ezulwini, yakishinikiza kuwepo kwa walau nafasi mbili za kudumu za Afrika kwenye baraza la usalama la UN.

Kando na uanachama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama, viongozi wa kiafrika pia wanaitisha mageuzi kwenye taasisi za kifedha za kimataifa, pamoja na mifumo ya ukopeshaji.

Wiki iliyopita, Marekani, mmoja wa wanachama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la UN ilisema kuwa inakubali kuwepo kwa viti viwili vya kudumu vya Afrika kwenye Baraza hilo lakini bila kura ya turufu. Hayo yakijiri, Nigeria inabaki kuwa na matumaini ya kupata moja wapo ya nafasi hizo.

Forum

XS
SM
MD
LG