Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 26, 2024 Local time: 00:29

Muhula wa pili wa rais Obama waanza


Rais Barack Obama aapishwa rasmi kwa muhula wa pili na Jaji mkuu John Roberts katika White House, Januari 20, 2013.
Rais Barack Obama aapishwa rasmi kwa muhula wa pili na Jaji mkuu John Roberts katika White House, Januari 20, 2013.
Rais Barack Obama aliapishwa rasmi Jumapili kuongoza Marekani kwa muhula wa pili wa miaka minne. Makamu rais wake Joe Biden pia aliapishwa.Tukio hilo muhimu litafanywa tena kwenye sherehe Jumatatu ambazo zinategemewa kushuhudiwa na maelfu ya watu katika uwanja mkuu wa kitaifa hapa jijini Washington DC.

Bwana Obama alikula kiapo saa chache kabla ya saa sita mchana Jumapili akiwa White House katika sherehe zilizochukua nusu dakika akiwa katika chumba cha Blu. Akiwa na mkewe Michele Obama na binti zake Malia na Sasha na kundi ndogo la waandishi habari, jaji mkuu John Roberts alimwapisha rais Obama kwa muhula wa pili.

Baada ya kula kiapo rais Obama alisalimiana na jaji huyo, na kuwapa busu mkewe na binti zake, akiwaambia, “nimefanya hivyo”.Hii ni mara ya saba katika historia ya Marekani kwa rais kula kiapo Jumapili kabla ya sherehe za umma Jumatatu inayofuata. Katiba ya Marekani inasema wazi kuwa muhula wa rais sharti uanze rasmi Januari 20 .

Bw. Obama alitumia Biblia iliyokuwa ya nyanya ya mkewe, LaVaughn Delores Robinson kula kiapo.Katika sherehe za umma baadaye leo Jumatatu nje ya majengo ya bunge, kwa mara nyingine tena atawekelea mikono yake kwenye Biblia iliyotumiwa na rais Abraham Lincoln alipoapishwa mwaka wa 1861. Bwana Obama atatumia Biblia ya pili, iliyomilikiwa na mtetezi wa haki za kiraia Martin Luther King Jr.

Sherehe za leo Jumatatu zitafanyika sambamba na siku kuu ya kitaifa ya Martin Luther King Jr. Mapema Jumapili, rais Obama na familia yake walihudhuria ibada katika kanisa la Metropolitan African Methodist Episcopal Church.

Naye makamu rais Joe Biden alikula kiapo cha kuhudumu muhula wa pili katika makao yake rasmi ya Naval Observatory hapa jijini Washington akitumia Biblia ya familia. Aliapishwa na jaji wa mahakama kuu Sonia Sotomayor na hii ni mara ya kwanza kwa jaji mwenye asili ya kihispania kumwapisha makamu rais wa Marekani.

Rais Obama anaanza muhula wake wa pili huku Wamarekani wakiwa na hisia mchanganyiko kuhusu hali ya kiuchumi, na uwezo wa viongozi wa vyama vyote viwili kuondoa tofauti zao za kisiasa na kutoa kipaumbele katika maswala ya kuongeza ajira na kutatua matatizo ya kifedha. Kauli mbiu ya rais Obama anapoapishwa kwa muhula wa pili ni ; “watu wetu,hali yetu ya baadaye.”

Wiki jana Ikulu ya White House ilitoa video ikiwa na ujumbe wa rais Obama akisema “nchi hii imepitia kipindi kigumu, lakini hatimaye tunaibuka tukiwa na nguvu zaidi“ tunaendelea kuimarisha muungano wetu kuhakikisha kila mtu anapata haki yake endapo atafanya bidii bila kujali anakotokea.”
XS
SM
MD
LG