Kuanzishwa kwa kituo kipya cha mpakani kati ya Kenya na Tanzania huko Lungalunga huenda ikachukua muda kabla marais wa mataifa hayo mawili kuzindua rasmi kituo hicho baada ya Tanzania kuomba muda kukamilisha ujenzi wa kituo hicho kwa upande wao.
Mipangilio ya kituo kimoja cha mpakani kati ya Kenya na Tanzania huko Lungalunga huenda kikachelewa kuanzishwa baada ya Tanzania kuomba muda zaidi kukamilisha upande wao.
Akizungumza na sauti ya Amerika afisa wa forodha anayesimamia kituo hicho upande wa Kenya Pius Sokoko Kwach amesema kuwa walipaswa kuanza shughuli za kituo kimoja mwezi huu wa tatu lakini Tanzania inachelewesha mpango huo.
Pius anasema “walituambia wanaweka mitandao yao sisi huku tuko tayari shuhuli katika kituo cha Kenya cha uhamiaji na forodha zinaendelea , hata upande wetu kitu chao kiko tayari ni wao wamalize kisha watuambie mara tu wakimaliza waje waianzishe kwani tayari tuko na tarakilishi tumishi zao ni wao waweke yetu upande wa Tanzania”.
Bw. Sokoko Kwach amekariri kuwa kituo hicho kitapunguza kucheleweshwa kwa shughuli za biashara na wasafiri wanaotumia mpaka huo kuenda na kutoka nchini Tanzania.
Pius anaendelea kusema “ maana na umuhimu ni kupunguza vituo vingi ambavyo vinasababisha ucheleweshaji shughuli hizi za one stop border ni kupunguza ucheleweshaji unaosababishwa na shughuli za kulipisha ushuru wa bidhaa na kuangalia wasafiri kati ya mpaka wa kenya na Tanzania.
Kampuni za mabasi zinazotumia mpaka wa Kenya na Tanzani kupitia Lungalunga zimekaribisha mipango hiyo ya kituo kimoja mpakani.
Yusuf Kassim ni msimamizi wa kampuni ya mabasi ya Tahmeed ya Mombasa - Daressalaam.
Aidha Yusuf ameitaka jumuiya ya Afrika Mashariki pia kufuatilia mbali swala la kadi ya ugonjwa wa manjano ambao unaendeleza rushwa hasa kwa wale ambao hawana kadi hizo wanapoingia ama kutoka Tanzania.
Bashiri Seif Saidi aliye dereva wa malori ya kusafirisha chakula cha msaada cha wakimbizi kutoka Mombasa hadi kituo cha wakimbizi cha Nyarugusu nchini Tanzania anasema bado wanalazimika kusubiri mpakani hata zaidi ya siku mbili kabla kuendelea na safari isipokuwa mpaka wa Rwanda na Tanzania.
Kituo sawia na hicho kinachounganisha kenya na Tanzania eneo la Taveta na Holili kilizinduliwa rasmi tarehe 27 mwezi Februari mwaka 2016 kama njia ya kuleta umoja katika jumuiya ya Afrika Mashariki.