Mazungumzo ya kutafuta amani Burundi yanayoendelea Arusha kaskazini mwa Tanzania chini ya Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamini mkapa yameingia katika siku ya tatu na ofisi ya msuluhishi huyo imetoa ufafanuzi kutokana na malalamiko ya baadhi ya wanaharakati ambao hawakualikwa.
Aidha ofisi hiyo imeeleza kwamba baadhi ya wadau muhimu katika mgogoro huo hawakuwasili kwenye mazungumzo ingawa wote wamealikwa.
Taarifa iliyotolewa na ofisi hiyo kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa wadau wote muhimu ikiwa ni pamoja na vyama vya upinzani, taasisi za kidini na wanaharakati wamealikwa na baadhi alithibitisha kushiriki na wengine hawakutoa majibu yoyote.
Taarifa hiyo imeanisha kwamba baadhi ya vyama vilivyoalikwa na ambavyo vimeweza kushiriki ni pamoja na CNDD /FDD ,Sahwanya Frodebu na Rodebu/ Copa pamoja marais wastaafu wa Burundi Sylvestre Ntibantunganya na Domitien Ndayizeye pamoja na mwanasiasa maarufu wa Burundi Agathon Ruasa .
Kwa mujibu wa taarifa hiyo vyama vilivyoalikwa na kushindwa kushiriki ni pamoja na chama cha MSD na kwa upande wa viongozi ni pamoja na Rais mstaafu wa Burundi Piere Buyoya na kwamba jitihada za kutafuta sababu za kushindwa kushiriki zinaendelea hadi sasa tayari wajumbe wawakilishi wapatao 83 wa makundi yenye masilahahi katika mgogoro huo wamefika Arusha na wanaendelea na majadiliano.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa mwishoni mwa juma awamu hiyo ya kwanza ya mazungumzo hayo inatarajiwa kuhitimishwa Jumanne.
Kwa upande mwengine mwishoni mwa wiki afisa wa cheo cha juu wa chama cha upinzani cha FNL Aime Magera anasema hana matumaini makubwa na matokeo ya mazungumzo hayo kwa vile anaamini serikali haitaki mazungumzo.