Ripoti Maalum Ajali Barabarani
Ajali za barabarani Afrika Mashariki zimekuwa moja ya majanga yanayogusa nchi hizo kwa kiwango kikubwa. Mwaka hadi mwaka idadi inaongezeka ya raia wanaopoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali za njia za usafiri. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani – WHO- ajali za barabarani na njia nyingine za usafiri katika bahari, maziwa na mito zinaendelea kusababisha vifo na madhara yanayobalidi maisha ya mtu milele. WHO inasema takriban watu milioni 1.25 hufariki kila mwaka kwa ajali ambazo zinaweza kuzuilika. Katika makala hii maalum, Idhaa ya Kiswahili ya VOA inaripoti kuhusu changamoto zinazokabili Afrika Mashariki, hususan Kenya, Tanzania na Uganda.
Tanzania
Asubuhi ya Jumamosi mei 6, 2017, basi dogo la shule likiwa limebeba watu 38 –wanafunzi wa shule ya msingi ya Lucky Vincent ya Arusha, Tanzania, na walimu wao liliserereka likiwa katika mteremko mkali karibu na mji wa Karatu, kaskazini mwa nchi hiyo na kuangukia mtaroni. Wanafunzi 32 walifariki papo hapo, pamoja na waalimu wao wawili na dereva.
Wanafunzi waliofariki walikuwa watoto wenye umri wa kati ya miaka 12 na 13. Walikuwa njiani kwenda kutembelea shule nyingine kufanya mtihani wa mazoezi. Watoto watatu tu ndio walionusurika na kusafirishwa hadi Marekani kwa matibabu. Ajali hiyo ilizusha masikitiko makubwa kote Afrika Mashariki –zaidi kutokana na umri mdogo wa waathirika. Rais John Magufuli wa Tanzania alisema ajali hiyo ilikuwa janga la kitaifa, kuongeza kuwa ajali hiyo imezima ndoto za watoto hao.
Ajali hiyo ilizusha masikitiko makubwa kote Afrika Mashariki –zaidi kutokana na umri mdogo wa waathirika. Rais John Magufuli wa Tanzania alisema ajali hiyo ilikuwa janga la kitaifa. Na kuelezea kuwa ajali hiyo imezima ndoto za watoto hao.
WHO inasema kwamba majeraha yanayotokana na ajli za barabarani ni sababu kuu ya vifo na ulemavu kwa watu duniani. Kulingana na utafiti wake wa mwaka 2016 kwa wastani watu watatu kati ya kila watu elfu 10 hupoteza maisha katika nchi hizo za Afrika Mashariki.Uganda inaongoza ikiwa na idadi kubwa zaidi ya wanaokufa kutokana na ajali hizo,ikifuatiwa na Tanzania, Rwanda, Kenya, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kenya
Nchini Kenya hadi kufika mwezi Mei mwaka 2017 idadi ya watu waliokufa katika ajali ilifikia 294 ukilinganisha na 269 waliofariki mpaka mwezi kama huu mwaka 2016.
Takwimu za Bodi ya Usalama wa Barabarani ya Kenya zinaonyesha pia waenda kwa miguu 451 wameuawa Kenya hadi kufikia mwezi Mei mwaka 2017
Nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, zina sheria zinazowataka madereva, hususan wanaoendesha malori au mabasi kwa muda mrefu, kupumzika kabla ya kuendelea na safari, lakini wachambuzi wanasema sheria hizo hazifuatwi na madereva wengi. Hali hii imetajwa kama moja ya sababu za ongezeko la ajali kwenye barabara za nchi hizo.
Uganda
Uganda nako, hali si nzuri pia. Miaka mitatu iliyopita (2014 mpaka 2016) Shirika la Afya Duniani liliitaja Uganda kuwa miongoni mwa nchi tatu za Afrika pamoja na Nigeria, na Afrika Kusini kama nchi zinazoongoza Afrika kwa ajali za barabarani.
Masaka road – barabara kuu inayotoka Kampala kwenda Kigali, Rwanda, inajulikana kama 'highway' ya ajali kutokana na wingi wa ajali mbaya zinazotokea katika barabara hiyo. Mwaka 2016 watu 200 walifariki katika barabara hiyo katika kipindi cha miezi sita tu.
Mkuu wa Polisi wa Usalama Barabarani nchini Uganda, Dr. Stephen Kasiimu ameizungumzia barabara ya Masaka ambayo inaelezewa hivi sasa nchini humo kuwa inachukua maisha ya watu wengi kutokana na ajali ambazo zinatokea kwenye barabara hiyo.