Wanajeshi wa Russia washambulia zaidi ya miji 40, Ukraine

Wanajeshi wa Ukraine wakiendesha kifaru katika mji wa Pokrovsk, Donetsk , Ukraine

Wanajeshi wa Russia wametekeleza mashambulizi katika zaidi ya miji 40, katika jimbo la Donbas, mashariki mwa Ukraine, na kuharibu nyumba nyingi.

Maafisa wamesema kwamba wanajeshi wa Russia, wanalenga kuwazingira wapiganaji wa Ukraine, na idadi yao imekuwa kubwa kuliko wa Ukraine katika baadhi ya sehemu.

Wanajeshi wa Russia wanajaribu kudhibithi Donbas kwa kuwasaidia wapiganaji wanaoungwa mkono na Russia, baada ya kushindwa kudhibithi mji mkuu wa Kyiv, au mji wa pili kwa ukubwa wa Kharkiv, kufuatia mapigano ya miezi mitatu.

Jimbo hilo lenye viwanda lina mikoa ya Luhansk na Donetsk.

Russia imetuma maelfu ya wanajeshi katika eneo hilo wanaoshambulia wapiganaji wa Ukraine kutoka kila upande katika miji ya Sievierodonetsk na, Lysychansk.

Mshauri wa wizara ya ndani ya Ukraine Vadym Denisenko amesema kwamba hali ni tete sasa Donbas wakati makundi 25 ya wanajeshi wa Russia wanajaribu kuwazingira wapiganaji wa Ukraine.