Ukame umesababisha ukosefu mkubwa wa chakula pembe ya Afrika

Boolo Aadan, 63, akiwa amembeba mjukuu wake wa umri wa miezi 9 katika kambi nje ya mji wa Mogadishu, Somalia, Feb. 4, 2022.

Serikali ya Somalia imesema kwamba zaidi ya watoto 300,000 wanakabiliwa na utapia mlo, na karibu raia wa Somalia 800,000 wamelazimika kuhama makwao kutokana na ukame ambao umeathiri pembe ya Afrika.

Rais Hassan Sheikh Mohamud, ameitembelea Baidoa, ambako wakaazi wameathiriwa sana na ukame.

Mjumbe maalum wa rais Mohamud, anayehusika na hali ya ukame na misaada ya kibinadamu, Abdirahman Abdishakur Warsame, amesema kwamba watu wanahitaji msaada wa dharura, na kwamba watoto wanahitaji msaada wa haraka.

Warsame, amesema kwamba Somalia haijapokea msaada wowote kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, na kwamba ana wasiwasi kwamba huenda hali ya ukame ikasababisha ukosefu mkubwa wa chakula.

Umoja wa mataifa umeonya kwamba pembe ya Afrika inakabiliwa na hali mbaya ya ukame kuwahi kuonekana katika muda wa miaka 40, kutokana na ukosefu wa mvua kwa misimu kadhaa.