Uchaguzi mkuu wa urais waanza leo Ufaransa

Wananchi wa Ufaransa wanapiga kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais.

- Uchaguzi mwaka huu hautabiriki

Upigaji Kura umeanza nchini kote Ufaransa katika moja ya chaguzi ambazo zinafuatiliwa kwa karibu sana baada ya miongo mingi pakiwepo wagombea 11, ambao kati yao ni wenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia na mrengo wa kushoto, wanaogombea nafasi ya urais Ufaransa.

Hali ya usalama imeimarishwa nchini humo baada ya shambulizi la kigaidi Jijini Paris siku kadhaa kabla ya uchaguzi ambapo mgombea mzalendo, dhidi ya Waislamu wenye siasa kali Marine Le Pen anaongoza katika kura za maoni.

Takriban maafisa polisi 50,000 wakisaidiwa na wanajeshi 7,000, vikiwemo vikosi maalum, vimepelekwa mitaani kwa ajili ya usalama baada ya kikundi cha kigaidi cha Islamic State kudai kimehusika na shambulizi la hivi karibuni.

Shambulizi hilo Alhamisi katika eneo maarufu la Champs-Elysees katikati ya Jiji la Paris lilimuua askari mmoja na kujeruhi watu wengine kadhaa.

Kura za maoni zafungwa

Emmanuel Macron amekuwa akiongoza katika kura za maoni, mgombea wa mrengo wa kati-kushoto ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Uchumi anaependelea Ufaransa iendelee kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya na anapendelea biashara pamoja na kuwa na mafungamano na chama cha Kisoshalisti kilichopoteza umaarufu cha Rais Francois Hollande.

Umaarufu wake uko hasa katika maeneo ya miji ilioshamiri kiuchumi nchini Ufaransa ambapo utandawazi umewanufaisha watu wengi.

Akimfuatia kwa karibu ni Le Pen, ambaye anataka kupiga marufuku uhamiaji nchini Ufaransa, hasa kutoka nchi za Kiislamu. Pia anataka Ufaransa kujitoa na Umoja wa Ulaya. Wafuasi wake wengi wako katika maeneo yaliokuwa na viwanda zamani nchini Ufaransa ambapo hivi sasa idadi kubwa ya watu hawana ajira na pia wanalaumu uchumi wa kisasa na mpango mzima wa jamii.

Mwanasiasa mwengine maarufu anaegombea ni Francois Fillon, ambaye anapendelea kupunguza matumizi ya umma na kushinikiza mageuzi makubwa katika Umoja wa Ulaya.

Uchaguzi hautabiriki

Wachambuzi wa kisiasa na wapiga kura waliohojiwa wanaona uchaguzi huu ni moja kati ya zile ambazo hazitabiriki tangia kumalizika kwa vita ya Pili ya Dunia. Katika wiki chache zilizopita kabla ya uchaguzi, mgombea wa mrengo wa kushoto zaidi Jean-Luc Melenchon alionyesha kuongoza katika kura za maoni na hivyo hivyo yalikuwa majadiliano ya mgombea huyo ambaye hakujitokeza siku za nyuma katika mitandao ya kijamii.

Kati ya vitu vilivyowavutia wapiga kura vijana ilikuwa kupitia mchezo wa video games uliotolewa ambapo mchezaji mmoja anajifanya ni Melenchon akitembea katika mitaa na kuchukua fedha kutoka kwa wanaume wenye kuvaa suti. Mchezaji huyo anaoneshwa akipambana na watu matajiri na wenye nguvu.

Hasira za wapiga kura

Hasira dhidi ya serikali zinafungamana na hisia zinazotawalia ushawishi unaoelekezwa kwa wapiga kura katika uchaguzi ambao suala la usalama, kuzorota kwa uchumi wa Ufaransa, kuporomoka kwa ajira kwa asilimia 10, na siasa kali za Kiislamu ni katika masuala yaliyoko katika fikra za wale wenye mrengo wa kushoto na kulia.

Hilo, wachambuzi wanasema, ndio shinikizo kwa kundi kubwa la watu, wakiwemo watu wa tabaka la kati na juu ambao ni wakazi wa Paris, katika kuchagua wagombea wenye msimamo mkali kama vile Le Pen na Melenchon.

“Baadhi yao kwa sababu ya hamasa. Huo ndio msingi wa uchaguzi, kama unavyofahamu. Ni kama kucheza nafasi ya roulette wa Russia, lakini kisiasa. Kwa wengine itakuwa kwa sababu wanachuki na wasomi wa nchi hii,” amesema Thomas Guénolé, mchambuzi wa mambo ya kisiasa huko Paris kuiambia VOA.

Washindi wawili wa duru ya kwanza ya uchaguzi wa Jumapili watachuana katika uchaguzi wa mwisho Mei 7. Upigaji kura utamalizika saa 1800 UTC.