Rais Biden: Mtoto wa kimarekani wa miaka minne aliyetekwa yuko Israel

Abigail Edan akizungumza na shangazi pamoja na mjomba wake katika Kituo cha Matibabu cha watoto cha Schneider kilichopo Israeli tarehe 27 Novemba 2023. Picha na Schneider Children's Medical Center of Israel/ REUTERS.

Msichana wa Kimarekani mwenye umri wa miaka minne yuko salama nchini Israel baada ya kuachiliwa siku ya Jumapili kutoka kwa waliokuwa wakimshikilia huko Gaza.

Rais wa Marekani Joe Biden alisema wakati alipokuwa akitaka kuongezwa muda wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas ili kuruhusu kuachiliwa kwa mateka zaidi.

"Yuko huru na sasa yuko Israel ," Biden aliwaambia waandishi wa habari muda mfupi baada ya jeshi la Israel kutangaza kuachiliwa kwa mateka 17 walikuwa wakiachiliwa na Hamas.

"Amepitia kiwewe kibaya sana” Biden alisema kuhusiana na mtoto, Abigail, ambaye wazazi wake waliuawa na wanamgambo wa Hamas wakati wanachama wa kundi la Kiislamu walipoishambulia Israel Oktoba 7.

Siku ya Ijumaa akiwa kifungoni, aliadhimisha miaka minne ya siku yake ya kuzaliwa, rais Biden alisema.

"Leo, yuko huru, Jill (Biden) na mimi, pamoja na Wamarekani wengi, tunamuombea kwa uhakika kwamba atakuwa sawa," alisema.

"Sasa yuko salama nchini Israel, na tunaendelea kushinikiza na kutarajia Wamarekani wengine wataachiliwa pia. Na hatutaacha kufanya kazi mpaka kila aliyetekwa amerejeshwa kwa wapendwa wao."
White House imesema kuwa Wamarekani 10 -- wanaume saba, wanawake wawili pamoja na Abigail – walitoweka na kudhaniwa wameshikiliwa mateka wa Hamas.