Mahakama moja inayohusiana na masuala ya uhamiaji hapa Marekani imempatia shangazi yake rais Barack Obama na hifadhi inayomruhusu kuendelea kuishi Marekani.
Zeytuni Onyango alihamia Marekani mwaka 2000 na alikuwa akiishi kinyume cha sheria tangu mwaka 2004 wakati jaji alipokataa ombi lake la kwanza la hifadhi ya kisiasa na kutoa amri ya kuondolewa nchini.
Wakili wa Onyango alitangaza Jumatatu kwamba ameruhusiwa kuishi Marekani. Taarifa za vyombo vya habari zinaripoti kwamba jaji alifikia uamuzi huo Ijumaa baada ya kusikiliza ushahidi Onyango katika mahakama ya Boston Massachusetts mwezi wa Febuari.
Kesi ya Bi.Onyango ilipata umashuhuri siku kadhaa kabla ya uchaguzi wa rais 2008. Wakati huo Bw.Obama alisema hakuwa na habari kwamba shangazi yake anaishi hapa nchini bila ya kibali cha halali, na alisema ni lazima sheria zote zinazostahiki zifuatwe.na kuheshimiwa.
White House na wakili wa Onyango wamesema kwamba Rais Obama hakuhusika kamwe katika kesi hiyo. Onyango ni dada wa kambo wa babake Obama.