Mubarak 'ahofia ghasia' akiondoka

Mpiga picha wa Ufaransa Alfred Yaghobzadeh akipewa matibabu na waandamanaji katika uwanja wa Tahrir Square, Cairo, Februari 2, 2011

Rais Hosni Mubarak wa Misri anasema angependa kujiuzulu madaraka mara moja lakini ana wasiwasi kuwa nchi hiyo itaiingia katika ghasia kubwa endapo atafanya hivyo.

Katika mahojiano yake ya kwanza Alhamisi tangu maandamano ya kupinga serikali yake kuanza aliambia televisheni ya ABC ya Marekani kuwa "amechoshwa" na madaraka.

Lakini alionya kuwa kundi lililopigwa marufuku la Muslim Brotherhood litachukua madaraka nchini humo endapo uongozi wake utaondoka hivi sasa.

Bwana Mubaraka alisema pia katika mahojiano hayo na mtangazaji Christan Amanpour kuwa serikali yake haihusiki hata kidogo na machafuko yaliyosababishwa na upinzani kati ya wafuasi wa Mubarak na wale wanaotaka aondoke madarakani.

Mji wa Cairo umeshuhudia siku nyingine ya mapambano kati ya pande hizo mbili. Waandishi wa habari kutoka mashirika mbali mbali ya nchi za magharibi pia wamekuwa wakishambuliwa katika siku mbili tatu zilizopita.