Baadhi ya mashirika ya ndege yamefuta au kubadilisha safari za ndege za kwenda Ukraine, huku kukiwa na hofu kubwa kwamba Russia huenda ikaivamia nchi hiyo jirani wakati wowote.
Hii ni licha ya mazungumzo ya ngazi ya juu ya mwishoni mwa wiki kati ya Kremlin na nchi za Magharibi, ikiwemo Marekani.
Shirika la ndege la Uholanzi KLM lilisema Jumamosi kwamba limefuta safari za ndege kwenda Ukraine hadi hali itakapotulia.
Nalo shirika la ndege la Ukraine la SkyUp, lilisema Jumapili kwamba safari yake kutoka Madeira, Ureno, hadi Kyiv, ilielekezwa katika mji mkuu wa Moldova, Chisinau, baada ya mkodishaji wa ndege hiyo, raia wa Ireland, kusema kuwa kampuni hiyo ilikuwa imepiga marufuku safari za ndege katika anga ya Ukraine.
Katika mazungumzo ya saa moja Jumamosi na Rais wa Russia Vladimir Putin, Rais wa Marekani Joe Biden alisema kuwa kuivamia Ukraine kutasababisha "mateso mengi ya binadamu" na kwamba nchi za magharibi zimejitolea kumaliza mgogoro huo kwa njia ya diplomasia.
“Hata hivyo, Biden aliongeza kwamba, wako tayari kwa lolote lile,” White House ilisema.
Taarifa hiyo ya ikulu haikuonyesha ishara zozozte kwamba mazungumzo hayo yalipunguza tishio la vita.
Marais hao wawili walizungumza siku moja baada ya mshauri wa usalama wa taifa wa Biden, Jake Sullivan, kuonya kwamba taarifa za kijasusi za Marekani zinaonyesha uvamizi wa Russia unaweza kuanza ndani ya siku chache.
Russia inakanusha kuwa ina nia ya kuvamia lakini imekusanya zaidi ya wanajeshi 100,000 karibu na mpaka wa Ukraine na imetuma wanajeshi kufanya mazoezi katika nchi jirani ya Belarus.
Maafisa wa Marekani wanasema kuwa Russia imeongeza nguvu zake za kijeshi na imefikia hatua ambayo inaweza kuvamia kwa haraka.