Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amewasili nchini Russia leo Jumanne ambako atafanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin katika mashariki ya mbali nchini Russia licha ya onyo la Marekani na Korea Kusini dhidi ya uwezekano mkubwa wa kuipa silaha Russia.
Maafisa wa Korea Kusini leo wamesema wanafuatilia kwa karibu mkutano huo wa kwanza kati ya Kim na Putin kufanyika katika kipindi cha miaka minne.
“Wizara ya ulinzi wa taifa inaamini kwamba Kim Jong Un huenda ameingia Russia mapema asubuhi akitumia treni binafsi,” amesema msemaji wa wizara ya ulinzi ya Korea Kusini Jeon Ha-Kyu, akitaja kuwepo kwa idadi kubwa ya wanajeshi ambao wamefuatana na Kim.
Ameongeza kuwa “wanafuatilia kwa karibu ikiwa mashauriano yanayohusiana na biashara ya silaha na uhamishaji wa teknolojia kati ya Korea Kaskazini na Russia yatafanyika.”