IFJ yaitaka Tanzania kumfutia mashtaka yote Kabendera

Umoja wa Waandishi wa Habari wa Kimataifa (IFJ) umeitaka serikali ya Tanzania kusitisha mashtaka yote dhidi ya mwandishi maarufu wa Tanzania Erick Kabendera kabla ya kufikishwa mahakamani Ijumaa.

Kabendera, mwandishi maarufu wa kujitegemea anayefanya kazi na vyombo vya habari ndani ya nchi na vya kimataifa, anashikiliwa rumande akisubiri kesi yake tangu Julai 29, wakati polisi walipomkamata na kumhoji juu ya uraia wake.

Lakini mara alipofikishwa mahakamani kwa ajili ya suala la dhamana yake Agosti 5, waendesha mashtaka walifungua kesi mpya na mashtaka tofauti ikiwemo kuwa katika mtandao wa wahalifu, ukwepaji kodi na utakatishaji fedha, makosa ambayo hayaruhusu mtuhumiwa kupewa dhamana.

Kesi ilipangwa kusikilizwa Agosti 19, lakini polisi waliomba tarehe ibadilishwe kuwa Agosti 30, wakisema walikuwa bado wanaendelea na uchunguzi.

IFJ imeeleza wasiwasi wake kuwa kukamatwa na mashtaka yanayotatanisha yenye tuhuma za uongo ni jaribio la kuficha kile ambacho ukweli ni ukatili wa kulipiza kisasi dhidi ya Kabendera kwa sababu ya uandishi wake.

“Amepelekwa mahakamani Jumatatu Agosti 5 lakini mashtaka yamebadilika kabisa na mpaka sasa hatujui iwapo suala la uraia na uchochezi vitaondolewa.

Pamoja na kuwa mawakili wake wamekuwa wanajaribu kupata pasipoti zote kutoka ofisi za uhamiaji, lakini maafisa wamekataa kutoa pasi hizo,” dada wa Kabendera amewaambia IFJ.

“Tunasubiri hatma ya kesi hiyo kesho mahakamani, kuona iwapo upande wa serikali utawasilisha ushahidi ili kesi ianze kusikilizwa au wataomba muda zaidi wakati Kabendera akiendelea kukaa jela,” ameongeza Prisca Kabendera.

IFJ inataka serikali ya Tanzania kumuondoshea mashtaka yote yaliyozuliwa dhidi ya Erick Kabendera na kumuachia mara moja.