Jumuiya ya kimataifa inaongeza shinikizo kwa kiongozi wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo wakati akijaribu kukabiliana na shambulizi la kijeshi la wapinzani wake.
Umoja wa Ulaya leo Jumatano iliwapiga marufuku wanachama wake kununua hisa za aina yoyote kutoka kwa serikali ya Gbagbo au kuipatia mikopo.
Sheria hiyo iliyopitishwa na baraza la Umoja wa Ulaya, inatoa ruhusa kwa ufadhili kwa ajili ya malengo ya kibinadamu. Awali Umoja wa Ulaya ilipiga marufuku ya usafiri na kuzuia mali za bwana Gbagbo na baadhi ya wafanyakazi wake. Leo Jumatano imemuongeza mtu mmoja kwenye orodha ya watu waliowekewa vikwazo hivyo.
Umoja wa Ulaya pamoja na Umoja wa Mataifa, jumuiya ya uchumi ya mataifa ya Afrika magharibi - ECOWAS wanamtaka bwana Gbagbo kukabidhi madaraka kwa mpinzani wake Alassane Ouattara, ambaye nchi nyingi zinamtambua kama mshindi wa uchaguzi wa Rais uliofanyika mwaka jana.
Wakati huo huo majeshi yanayomuunga mkono Rais wa Ivory Coast anayetambulika kimataifa, Alassane Ouattara, yameshambulia nyumba ya kiongozi Laurent Gbagbo anayeng’ang’ania madaraka katika jitihada za kumlazimisha ajisalimishe.
Mashahidi wanaripoti kusikia milio silaha nzito kuzunguka makazi mjini Abidjan, mahali ambapo bwana Gbagbo amejificha kwenye handaki moja la chini ya ardhi na familia yake.