Jenerali Burhan ajiteua mwenyewe kuwa kiongozi wa mpito wa Sudan

Jenerali Abdel-Fattah Burhan

Kiongozi wa mapinduzi nchini Sudan Abdel Fattah al-Burhan ametangaza baraza jipya la uongozi akiwa kiongozi na kuwaacha wajumbe wa kiraia wa baraza lililopita. 

Jenerali Burhan alikula kiapo jana na amembakisha naibu wake Mohamed Hamdan DSagalo, ambaye anajulikana kama Hemeti na viongozi wengine wa juu wa jeshi katika nafasi zao walizokuwa wameshikilia kabla ya mapinduzi ya Oktoba 25. Baraza hilo lenye wajumbe 14 pia linajumuisha raia wengine lakini hakuna aliyekuwa katika ushirikiano wa kisiasa aliyekuwepo katika madaraka kabla ya mapinduzi.

Waziri wa Habari aliyekuwa katika serikali iliyotimuliwa Hamza Balloul ameueleza uamuzi huo kuwa ni hatua nyingine ya kuongeza muda wa mapinduzi na kusema kuwa wananchi wanaweza kuwashinda na kuendelea na kipindi cha mpito.

Baraza jipya limetangazwa wakati ambapo kuna shinikizo la ndani na kimataifa kubadilisha mapinduzi. Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Sudan, Volker Perthes amesema kwamba uteuzi wake wa peke yake wa baraza hilo unafanya hali kuwa ngumu zaidi kwa nchi hiyo kurejea katika utawala wa kikatiba.