Biden, Putin wazungumzia kupunguza mgogoro wa Ukraine

Rais wa Marekani Joe Biden akiwa katika mazungumzo na Rais wa Russia Vladimir Putin kutoka nyumbani kwake huko Wilmington, Delaware, Marekani Disemba 30, 2021. Adam Schultz/White House/Handout via REUTERS

Kwa mara ya pili katika mwezi huu, Rais wa Marekani Joe Biden amezungumza moja kwa moja na mwenzake wa Russia na kumsihi apunguze matendo yake, huku Rais Vladimir Putin akiendelea kuongeza idadi ya wanajeshi karibu na mpaka na Ukraine.

Lakini maafisa wa utawala walisema Putin hakutoa uhakikisho kuhusu azma yake.

Na sasa katika duru ya pili, Rais wa Marekani Joe Biden mara mwisho alizungumza na Rais wa Russia, Vladimiri Putin chini ya mwezi mmoja uliopita.

Wawili hao walizungumza tena Alhamisi, Biden alimsihi Putin kupunguza mivutano na Ukraine, White House ilisema mazungumzo hayo kwa njia ya simu yalidumu kwa dakika 50.

Mambo mengi yalijitokeza katika mazungumzo hayo ya simu huku kiongozi wa Russia akiendelea kukusanya maelfu ya wanajeshi kwenye mpaka na Ukraine, kama inavyoonekana katika kanda ya video iliyotolewa wiki iliyopita na wizara ya ulinzi ya Russia.

Maafisa wa utawala wa Biden wamesema kwamba wawili hao walikuwa na majadiliano mazito na muhimu. Lakini afisa mwandamizi wa utawala alisema alipoulizwa, kwamba Putin hakusema lolote kuhusu azma zake. Maafisa wa ngazi ya juu kutoka mataifa hayo mawili watakutana tena mapema mwezi Januari mjini Geneva, bila ya marais hao wawili.

FILE - Rais wa Ukrainian Volodymyr Zelenskiy akitembelea majeshi yaliyoko mstari wa mbele upande wa mashariki wa Ukraine, April 9, 2021, ambapo waasi wanaoungwa mkono na Russia wanapambana na majeshi ya Ukraine katika mgogoro wa tangu 2014 uliouwa zaidi ya watu 14,000 .

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, alitweet siku ya Jumatano kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken aliapa “msaada kamili wa Marekani kwa Ukraine ili kukabiliana na uchokozi wa Russia.”

Mapema mwezi December, alilitembelea eneo la mstari wa mbele na kusema wanajeshi wake wako tayari.

Ingawaje wachamabuzi wanaonekana kuwa na mashaka kuwa Putin anaweza kuivamia Ukraine, wana wasi wasi kwamba maelfu ya wanajeshi waliopelekwa kwenye eneo hilo huenda kwa bahati mbaya au kwa makusudi wakachochea vita.

Will Pomeranz, wa Kituo cha Wilson Center anaeleza: “Kama anadanganya, basi hili linatia wasi wasi mkubwa sana ambao hasa ni hatari kwa Putin kwasabay lazima ahakikishe kwamba wanajeshi 100,000 na zaidi walioko huko hawatachukua hatua zozote wao wenyewe kabla ya kupewa amri. Kwahiyo nadhani hali hiyo kwa kweli inatisha yenye maafa kwa pande zote mbili.”

Je nini kitatokea hivi sasa?

White House imesema na imerejea kusisitiza, kwamba kutakuwa na “madhara makubwa” kama Russia ikivamia, ikiwa ni pamoja vikwazo vikali sana vya kiuchumi na kuongeza msaada wa ulinzi kwa Ukraine. Lakini baadhi ya wachambuizi wanasema Putin anajionyesha tu.

Leon Aron, wa Taasisi ya American Enterprise anasema :“Putin kwa mafanikio anasababisha dhana ya dharura. Kama ukiangalia, lugha inayojitokeza ni ile ile. Anatarajia kuanzisha vita, anaweza kuivamia Ukraine. Kwa hakika, White House inaliangalia hilo. Mimi hapana, kwasababu, kama nilivyoandika na nilipozungumzia kuhusu hili, Putin hataivamia Ukraine wakati huu. Anacheza mchezo wa kuwaonyesha nyumbani kwake. Na yote haya ni sehemu ya mchezo ambao Putin anaucheza, nadhani ataendelea kuucheza, walau mpaka uchaguzi wa mwaka 2024.”

Duru ijayo ya mazungumzo ya pamoja itaanza Januari 10 mjini Geneva, je mambo yatakuwa kimya kwa upande wa Ukraine?