Rais wa Marekani Joe Biden kwa mara nyingine amemuonya Rais wa Russia Vladimir Putin katika mazungumzo ya simu Jumamosi kuhusu “uharaka na ukubwa” wa matokeo hasi iwapo Russia itaivamia Ukraine, kulingana na taarifa kutoka White House.
Biden na Putin walijadili mgogoro huo wakati mivutano ikiendelea kukua katikati ya wasiwasi uliopo kwamba Russia iko tayari kufanya uvamizi kwa Ukraine.
Russia imeendelea kuongeza wanajeshi wa ziada kuliko idadi ya awali ya wanajeshi 100,000 waliopelekwa katika mpaka wa Ukraine katika miezi ya karibuni.
Baada ya mazungumzo, Yuri Ushakov, mshauri wa juu wa Kremlin wa sera za mambo ya nje, alisema Biden kwa kiasi kikubwa alirejea fikra alizotoa Januari kujibu masuala ya usalama yanayoitia wasiwasi Russia.
“Lakini kwa bahati mbaya, na hili lilisemwa, haya mapendekezo hayagusi vitu muhimu vya msingi vya juhudi za Russia,” afisa huyo wa Kremlin alisema.
Aliongeza kuwa Russia itajibu mapendekezo ya upande wa pili karibuni.
Ushakov alisema wito huo ulikuwa “hauegemei upande mmoja na kama wakibiashara” na viongozi hao wawili “wamekubaliana kuendeleza mawasiliano katika ngazi zote.
Lakini pia alikerwa na taarifa za Marekani kwamba uvamizi huo ungetokea karibuni, akisema: “Hofu imefikia kileleni.”
Washington imepokea taarifa za kipelelezi kuwa uvamizi huo ungeweza kutokea mapema pengine siku ya Jumatano.
White House imesema Biden alifanya mazungumzo ya simu kutokea Camp David, Maryland, kuanzia saa 11:04 am EST hadi saa 12:06 p.m. EST.