Naibu kamishna wa wilaya ya Ghotki Mohammed Usman Abdullah nchini Pakistan anasema idadi ya watu waliojeruhiwa kutokana na ajali ya treni kusini mwa nchi imeongezeka kupindukia 100 na karibu watu 38 wamefariki.
Akizungumza na waandishi habari Abdullah amesema wafanyakazi wa uokozi wanaendelea kujaribu kuwaondoa abiria waliokwama ndani ya mabaki ya treni na huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka.
Maafisa wa usafiri wa reli wanasema kulikuwepo na zaidi ya watu elfu moja ndani ya treni mbili zilizogongana baada ya kwanza kuanguka kutoka katika njia ya reli.
Waziri wa Habari wa Pakistan Fawad Chaudhry amesema kwenye taarifa ni mapema kusema ikiwa ajali hiyo imetokana na matatizo ya kiufundi, uzembe au uharibifu wa maksudi akiongeza kwamba uchunguzi kamili utafanyika.