Waislamu waridhika na hotuba ya Obama

Rais Barack Obama amesema baada ya miongo kadhaa ya kukereka na kutoaminiana huu ni wakati wa kuanza majadiliano na mwanzo mpya.

"Nimekuja hapa Cairo kutafuta mwanzo mpya kati ya Marekani na Waislamu kote duniani, kwa msingi wa maslahi ya pamoja na kuheshimiana na wenye msingi wa ukweli kwamba Marekani na Uislamu hazitengani na hamna haja ya kushindana"

Ingawa alitoa hotuba yake kwenye ukumbi mkubwa kabisa ulojaa watu katika chuo kikuu cha Cairo, alikua na lengo hasa ya kuzungumza na zaidi waislamu bilioni moja duniani. Rais Obama alisema ni lazima matatizo yatanzuliwe kwa ushirikiano na mivutano inabidi ikabiliwe moja kwa moja.

Hotuba hiyo imepokelewa vyema katika kila pembe ya dunia wengi wakisema ni hatua muhimu ya kuanza majadiliano lakini kunahitajika vitendo kabla ya kuweza kuaminika kwamba serekali ya Marekani inataka kuleta mabadiliko.

Tumezungumza na watu mbali mbali huko Mashariki ya Kati na Afrika Mashariki na wameelza kwa kiwango kikubwa wameridhika na hotuba hiyo.