Miezi mitatu tangu achukue uongozi, Rais John Magufuli wa Tanzania anaendelea kufanya mageuzi katika utendaji wa kazi nchini humo hasa katika kuwaajibisha maafisa watendaji wakuu serikalini na idara za umma. Katika muda wa siku tatu zilizopita Magufuli amesimamisha kazi maafisa sita wa ngazi za juu.
Ikulu ya Dar es salaam ilitangaza hatua nyingine mpya Jumatatu ambapo Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa -NIDA, Dickson Maimu na watumishi wengine wanne wa mamlaka hiyo ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha kiasi cha shilingi bilioni 179.6 zilizotumika mpaka sasa katika mradi wa vitambulisho vya taifa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita kiongozi huyo aliwasimamisha kazi maafisa wawili waandamizi wa idara ya uhamiaji kwa madai ya utendaji mbaya wa kazi na ubadhirifu wa fedha.
Katibu kiongozi wa Ikulu, Balozi Ombeni Sefue, alisema katika mkutano na waandishi wa habari Dar es salaam Jumatatu kuwa Rais Magufuli anataka uchunguzi ufanyike kutokana na fedha nyingi kutumiwa wakati sehemu kubwa ya wananchi hawajapata vitambulisho.
Msemaji wa Rais Gerson Msigwa aliambia VOA wiki iliyopita kuwa hatua ya kuwasimamisha kazi maafisa waandamizi ni sehemu ya ahadi ya kampeni ya Rais Magufuli kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na viongozi walio safi na wenye maadili.
Tangu aiingie madarakani Rais Magufuli amechukua hatua kadha kuleta utendaji bora serikali ikiwa ni pamoja na kuwataka makatibu wakuu wapya mapema mwezi huu kutia saini hadharani hati ya uadilifu katika utendaji wao wa kazi.
Katika hatua nyingine zilizotangazwa na Balozi Sefue Jumatatu Rais Magufuli amefanya mabadiliko kadha kwenye balozi za nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwarudisha nyumbani mabalozi waliomaliza muda wao nje ya nchi, wakiwemo Batilda Burian kutoka Tokyo, Japan na Dk. James Nsekela kutoka Roma, Italia. Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Peter Kallaghe tayari amerejeshwa Tanzania ambapo atapangiwa kazi nyingine.
Wapinzani wamekuwa wakidai kuwa hatua za Rais Magufuli ni “maonyesho” tu kuwa anafanya kazi kama ahadi yake ya kampeni ilivyosema, lakini maafisa wa Ikulu hatua hizo zinalenga kutekeleza ahadi ya kuboresha uchumi, kuongeza nafasi za kazi, kupambana na rushwa na kuhakikisha sekta za umma zinafanya kazi kuboresha kiwango cha maisha ya wananchi.