Mpinzani wake mkuu ambaye pia ni kaimu waziri mkuu Yair Lapid, pamoja na mke wake wamepiga kura mapema Jumanne mjini Tel Aviv. Netanyahu ambaye kwa sasa ni kiongozi wa upinzani amekamilisha kampeni yake kuelekea kwenye uchaguzi huo wakati akikabiliwa na mashitaka ya tuhuma za ufisadi.
Mgombea mwingine ambaye amepata umaarufu mkubwa kwenye utafiti wa maoni katika siku za karibuni ni Ben Gvir, ambaye ni mwanasiasa wa mrengo mkali wa kulia. Utafiti huo unaonesha matokeo huwenda yakawa sawa na uchaguzi uliyopita ambapo hakuna upande utaweza kutawala kwa urahisi.
Kutokana na migawanyiko mikubwa kwenye siasa za Israel, wote Lapid na Netanyahu hawatarajiwi kupata wingi wa moja kwa moja kwenye bunge la Knesset lenye wajumbe 120.
Hilo lina maana kwamba watageukia uungaji mkono wa vyama vidogo vya kisiasa, kwa matumaini ya kupata viti 61 vya bunge vinavyo hitajika ili kuunda serikali. Kura za maoni zinaonyesha ushindani mkubwa kati ya wagombea, na kwa hivyo kuwa vigumu kutabiri mshindi.