Iwacu imeongeza kuwa dereva wake aliyekuwa anashutumiwa pamoja na wanahabari hao yeye amekutwa hana hatia na ameachiwa huru. Mahakama imeomba pia wanahabari hao kulipa faini ya faranga milioni 1 za Burundi, sawa na dola za Marekani 529.
Mkurungezi wa gazeti hilo, Antoine Kaburahe ameitaja hukumu hiyo kama aibu kwa vyombo vya sheria nchini humo.
“Sisi tunafikiri majaji wamepewa shinikizo la kutowaachia huru wanahabari wetu. Ukitizama uzito wa kosa wanalotuhumiwa la kutaka kuvuruga usalama wa taifa, haileweki kuona wamepewa hukumu ndogo kama hiyo,” Kaburahe ameiambia Sauti ya Amerika.
“Majaji wameshindwa kutekeleza wajibu wao wa kutenda haki," ameongeza. Kaburahe amesema watakata rufaa.
Wanahabari Christine Kamikazi, Agnes Ndirubusa, Terence Mpozenzi na Egide Harerimana walikamatwa tarehe 22 Oktoba mwaka 2019 katika mkoa wa kaskazini magharibi mwa Burundi wa Bubanza, wakienda kuripoti kuhusu mapigano yaliotokea katika eneo hilo.
Polisi iliwakamata na kuwafikisha mbele ya muendesha mashtaka, ambaye aliwafungulia mashtaka ya kutaka kuhatarisha usalama wa taifa. Wakati wa kusikilizwa kesi mwishoni mwa mwezi Disemba 2019, mwendesha mashtaka aliiomba mahakama iwape kifungo cha miaka 15.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.